29/06/2017
HISTORIA YA WANYATURU.
WANYATURU ambao awali walijulikana kwa jina la Warimi ni watu wanaoishi karibu wilaya zote za mkoa wa Singida yenye wilaya saba.
Kwa Mujibu wa Patrick Mdachi katika kitabu cha Wanyaturu wa Singida, Mila na Desturi zao, Wanyaturu ni moja ya makabila yanayojumlishwa katika kundi la Nilo-Hamites, lenye asili ya Wabantu walioishi Abysinia ambayo sasa inajulikana k**a nchi ya Ethiopia.
Watu hao waliihama Abysinia (Ethiopia) kutokana na njaa kubwa kiasi ambacho hawakuweza kustahimili kukaa tena hapo. Njaa ndiyo iliwalazimisha watu hao kufikia kula nzige, katika harakati za kutafuta nzige hao ndio ukawa mwanzo wa safari yao ya kuhama.
Mdachi anasema katika kitabu chake hicho kilichochapishwa na Benedictine Publicationss Nandanda - Peramiho mwaka 1991, kuwa Wanyaturu waliingia Tanzania kupitia sehemu ya kaskazini kutokea Kenya na Uganda na kufanya maskani yao eneo la Uzinza, Mwanza, baadaye walihamia eneo la Pasiansi na mwaka 1700 walikutwa na Wasukuma ambao waliwafukuza na kuwafanya wakimbilie Ntunzu.
Baadhi ya watu hao (yaani Mwilwana na Masanja) wakiwa na wake zao na watu wengine wa kuwasaidia kazi hawakuweza kukaa Ntunzu, waliendelea na safari pamoja na ng’ombe wao mpaka mkoani Singida, eneo la mashariki lijulikanalo k**a Sepuka.
Mdachi anasimulia kwamba Wanyaturu hao walikaa hapo kidogo na ndio eneo hilo ambalo watu hao waligawanyika tena, lengo likiwa ni kupeana nafasi ya kilimo, ufugaji na kuweka makazi ya kudumu. Mwilwana akielekea kaskazinimashariki eneo la Ilongero ambapo alistawisha makao yake hapo na hapo ukawa mwanzo wa Mwilwana huku Masanja akienda upande wa mashariki eneo la Kisaki na kujenga juu ya jiwe liitwalo Wahi, anasimulia Mdachi.
Kwa mujibu wa masimulizi hayo, Masanja alijaaliwa kuwa na watoto wanne ambao aliwapa majina yao kulingana na kazi walizofanya au tabia. Watoto hao ni Sengasenga aliyepewa jina hilo kutokana na kuwa baba yao alipoanza akiwa maskani alifyeka mapori. Kufyeka pori kwa Kinyaturu ni ‘Usenga’.
Mtoto mwingine aliyefuatia aliitwa Mpuma ambaye alipewa jina hilo kutokana na eneo hilo kuwa na tumbili wengi. Mpuma kwa Kinyaturu ni tumbili. Mtoto wa tatu alipewa jina la Hati kutokana na jiwe ambalo baba yao alitumia kujenga nyumba na wa mwisho alijulikana kwa jina la Mkahiu kutokana na furaha ya wazazi wao.
Watoto hawa walitawanyika ikiwa ni suluhu ya ugomvi wao na kila mmoja alianzisha ukoo wake ambazo zilikuja kujulikana k**a Senga, Anyahati, Puma na Ukahiu. Utafiti unaonesha kuwa jina la kabila la Wanyaturu ni la hivi karibuni, awali kabila hili lilijulikana k**a Warimi. Jina hilo walipewa na watani wao Wanyamwezi ambao walikuwa wakiwinda pamoja.
Siku moja wakiwa katika kuwinda walimpiga mshale wa sumu mnyama wa porini, mnyama huyo akakimbia na Wanyaturu wakiwa wanamkimbiza walikuwa wakisema ‘Mughuu turu, turu’ wakimaanisha mguu huu hapa.
Wanyamwezi wakaanza kuwaita Banyaturu jina likaendelea kukolea mpaka leo wanaitwa kwa jina hilo na lile lao la asili, yaani Warimi, likapotea. Wanyaturu ni watu wanaopakana na makabila ya Wanyiramba na Winyisanzu (magharibi), Wamang’ati ambao pia huitwa Wabarbaig (kaskazini-mashariki), Wasandawe (mashariki), Wagogo (kusini) na Wanyamwezi na Wasukuma upande wa Kusinimagharibi.
Muundo wa utawala wa Wanyaturu Mfumo wa utawala wa kisiasa wa kabla na baada ya kuingia wakoloni unahusu imani na utaratibu wa dini za kiasili. Tofauti na makabila mengi hapa nchini, Wanyaturu hawakuwa na utawala wa kichifu. Katika kabila hili kila ukoo ulikuwa na wazee (ambao kwa siku hizi tungewaita halmashauri) ambao kazi yao kubwa ilikuwa ni kushauri pamoja na kupatanisha mashauri mbalimbali.
Koo zinapokuwa nyingi zilipata kiongozi mmoja ambaye alichaguliwa kutokana na kazi yake, pamoja na ujasiri wake wa kivita. Uongozi wa namna hiyo haukuwa wa kurithi, bali ulipatikana k**a Wanyaturu wanaovyoamini hutokana na bahati au neema ya jua.
Jinsi kiongozi anavyopatikana husemakana kuwa na nyota ya pekee sana hasa kutokana na kuwa na waganga au waaguzi ambao humsaidia katika kazi zake. Waaguzi hao ambao huchaguliwa kutoka kwenye ndoto na uteuzi wake hujulishwa na miungu au mungu mwenyewe na kazi yao kubwa ilikuwa ni kutabiri mambo ya baadaye katika jamii.
Hivyo kumfanya kiongozi kutekeleza mambo yake kwa mwongozo wa ndoto za waganga hao. Waaguzi hao ndio waliokuwa viongozi wa kiroho. Kila kiongozi wa kivita alikuwa na kiongozi wake wa kiroho ambaye pia alikuwa akimpa dawa za kinga. Mganga au muuguzi mkuu alikuwa akiitwa Saigiro ambaye inasemekana alikuwa akitoka kabila la Tatong.
Ujio wa wakoloni Stanley alionekana katika eneo la Wanyaturu mwaka 1874 baada ya kuweka bomba na chuma juu ya jiwe la Damankia, eneo la Dung’unyi, katika tarafa ya Ikungi. Stanley alitanguliwa na Waarabu ambao inasemakana walikuwa wa kwanza kukanyaga ardhi ya Wanyaturu. Hawa walikwenda kutafuta mtama.
Watu hao wote waliwaona Wanyaturu kuwa ni watu wanaopenda vita. Mwaka 1900 ndio mwaka ambao Wajerumani walianza kuingia taratibu na mbinu waliyoitumia kuingia ilikuwa ni kwa kuwavutia viongozi wa vita ambao walikwenda k**a wajumbe wa biashara ya ng’ombe na mtama kwa nguo na shanga.
Hata hivyo, ujio wa wakoloni, ulitabiriwa na mganga Sakilo ambaye aliishi katika mlima Hanah na ambaye alikuwa aidha anatoka katika kabila la Tatog au Kimbugwe ambao walitabiri ujio wa wekundu wasio na vidole miguuni, kwani walivaa viatu. Jina lingine walilopewa wazungu na Wanyaturu ni ‘Anyeke’, yaani watu walio na miguu k**a tunda bivu kutokana na kuvaa viatu.
Baadhi ya Wanyaturu hawaukufuatilia utabiri huo kutokana na kupendelea sana utabiri wa Mahindi wa Isuna ambaye alitabiri kuwa Maksai mwekundu alionekana katika maamkio yake na kukatokea vifo vingi, njaa, vitisho na fujo za kila namna. Kwa Wanyaturu rangi nyekundu ni hatari na ng’ombe mwekundu huwa hatumiki kwenye sadaka ya aina yoyote.
Karibu Singida.
_________👇____________
HISTORIA YA WANYATURU II.
Wanyaturu (au Waturu ; wao hupendelea kuitwa Arimi, yaani watu wa Rimi ni kabila la watu wa
Tanzania wanaoishi katika Mkoa wa Singida .
Lugha yao ni Kinyaturu, ambacho ni jamii ya Kibantu, lakini kina fonimu nyingi za Kikushi .
Historia
Asili ya kabila hilo inasemekana ni nchi ya Ethiopia ambako kunasadikiwa kuwa na watu wanaotumia lugha ambayo kwa asilimia kubwa inafanana na Kinyaturu. Hudhaniwa pia kuwa Wanyaturu na Wakushi wa Ethiopia asili yao ni moja.
Walipoingia eneo la Tanganyika walichangamana na Wanyatunzu pamoja na Wasukuma , ndiyo maana
mila na tamaduni zao zinashabihiana kwa kiasi kikubwa, hivi kwamba ni vigumu kumpambanua Mnyaturu baina ya Wanyatunzu.
Wana utani na Wanyiramba na
Wairaqw .
Idadi na mgawanyiko
Mwaka 1993 walikuwa 556,000 .
Ndani ya kabila hilo, kuna makundi matatu:
Vahi (Wahi) , ambao ni zaidi ya nusu ya Wanyaturu wote, na kuwa wenyeji wa mji wa Singida : hao wanaishi kuanzia Singida mjini hadi karibu na
wilaya ya Manyoni.
Airwana (Wilwana) wanaishi
kaskazini kwa ziwa Singida;
na lile dogo zaidi la Anyiŋanyi (Wanyinganyi) wanaoishi maeneo ya
Mnying'anyi .
Unyambwa pia ni sehemu iliyoko Singida na inasemekana ni ukoo mkubwa sana wenye mababu wakubwa wawili: mzee Ghambona na Hante. Ukoo huu hauvumi sana kutokana na watoto wa wazee hao kuhama Unyambwa na kwenda Iguguno, ambako lakini hawakukaa sana, wakahama tena na kuelekea hasa mikoa jirani k**a Shinyanga , Tabora na Mwanza . Ni ukoo wenye watoto wengi wa k**e kuliko wa kiume, na dini yao kubwa ni Uislamu .
Tanbihi
1. ↑ Pengine jina "Wanyaturu" linapoteza historia yao kwani liliundwa na Wazungu
2. ↑ Unaweza kubadilisha hapa kuhusu Airwana kuwa si wengi karibu nusu ya Wanyaturu wote kwa ukianzia pale mjini Singida ukielekea Kusini hadi sehemu za Issuna hadi Itigi na Manyoni hadi Kintinku hawa ni Vahi tu, bado sijasema sehemu za Ihanja hadi Muhintiri na sehemu za Mang'onyi na Misughaa ni vahi au wahi kwa hiyo robo tatu ya wanyaturu ni wahi yaani vahi waweza kufanya utafiti na utagundua ukweli huo. wairwana wana maeneo kuelekea Kaskazini ambayo ni sehemu ndogo sana kieneo na inapakana na Wanyiramba ukifika sehemu za Iguguno.
Tukiangalia asili ya kabila la Wanyaturu, utawala wao na ujio wa wakoloni kwa mujibu wa Patrick Mdachi katika kitabu chake cha Wanyaturu wa Singida, Mila na Desturi zao.
Kwa kifupi anasema kwamba Wanyaturu ni moja ya makabila yanayojumlishwa katika kundi la Nilo-Hamites, lenye asili ya Wabantu walioishi Abysinia ambayo sasa inajulikana k**a nchi ya Ethiopia. Leo tunaendelea na simulizi la kabila hilo kwa mujibu wa Mdachi katika kitabu hicho kilichochapishwa na Benedictine Publications Nandanda - Peramiho mwaka 1991.
Mdachi anaendelea kusimulia kwamba Wakoloni wa Kijerumani hawakuweza kuingia kirahisi katika ardhi ya Wanyaturu. Ujio wao kuliibua mvutano ambao ulitokea na kuenea sehemu za Iramba na Isanzu kutokana na jamii kutokubaliana na mfumo mpya wa siasa, jambo lililowafanya kugoma, mgomo uliotokea mwaka 1902.
Uchumi wa sehemu ya kusini mwa Singida ulitegemea ng’ombe pamoja na mtama. Wajerumani walijitahidi kubadilisha hali ya uchumi na kuleta hali mpya ya uchumi baada tu ya kuanzishwa msh*tuko katika maisha ya jamii. Hali hii ndiyo iliyofanya kuwapo kwa mgomo mkali kusini kuliko sehemu ya kaskazini.
Wanyaturu waliwachukia Wajerumani kwa sababu ya unyang’anyi wao na kuwaweka nguvuni baadhi ya viongozi wa kivita.Lingine lililowaudhi ni kuanzishwa kwa ukusanyaji wa kodi na kuanzisha matumizi ya sarafu ya mviringo iliyopigwa chapa ya Kilimatinde mwaka 1907. Kuna wengine walipinga hatua ya kuwapa nguo na kubadilishana kwa ng’ombe.
Katika kuonesha kuwa nguo hizo hazina thamani kwao, Wanyaturu wakazilinganisha na kuku kwamba ni sawa na mtu kumpa ng’ombe yeye akakupa kuku, Mdachi anasimulia. Katika mapambano hayo, Wanyaturu walionekana ni jasiri kutokana na jeuri iliyotokana na Mungu wa mvua ‘Tita’ na kuongozwa na utabiri.
Mbinu za Wanyaturu katika vita hii zilikuwa ni zile za maficho (porini) huku wakitumia mishale. Mathalani, majumbe walijikuta wamezingirwa kwenye duara na watu wenye mikuki yenye kutisha, matokeo ilikuwa ni kutolipwa kwa kodi na ilibidi wakusanyaji kodi watoe wenyewe kodi hizo ambapo walizilipiza kwa wanyonge zaidi.
Mfano mzuri wa mgomo wa Wanyaturu katika eneo la Wilwana, ni mwanamke aliyejulikana kwa jila na Leti wa Ughandi kuongoza mgomo wa Wanyaturu sehemu ya kaskazini. Alipinga utawala wa aina yoyote ule kutoka nje, hivyo kwa kutumia nguvu na msimamo wake alifuatwa na jeshi la Wakoloni, lakini kwa akili zake aliweza kutumia nyuki kulifukuza jeshi hilo.
Alichokuwa akifanya ni kwa kutumia nguvu zake aliweza kuwakusanya nyuki pamoja na hawa wakoloni walipotokea aliwafungulia nyuki ambao walishambulia na kulazimika kukimbia. Hata hivyo, kwa kutumia mbinu za kuzingira na kuteka nyara baadaye alishindwa kutokana na Wajerumani kutumia silaha za kisasa zaidi, yaani bunduki dhidi ya silaha zake za nyuki.
Maisha Kwa Wanyaturu mwanamke ana majukumu mengi katika jamii ikiwa ni pamoja na kulima, kuvuna, kupiga mtama, kuchanja kuni, kazi za jikoni. Kutokana na miiko, kazi kwa mwanamke mjamzito hupungua kwani anatengewa muda mwingi wa kupumzika hivyo kubakia na kazi ya jikoni na zingine ndogondogo.
Miiko kwa upande wa vyakula, mjamzito alikuwa haruhusiwi kula mayai (kwa dhana kuwa atazaa mtoto asiye na nywele) na pia hakuruhusiwa kunywa pombe kali (pombe ya asili), lakini vyakula vingine aliweza kula bila tatizo lolote. Baada ya kujifungua mama hupewa wasaidizi wa kazi na wengine wa kumkanda tumbo.
Muda huo mume hutayarisha mbuzi beberu ambalo huchinjwa na humpatia mkewe mchuzi (supu) k**a pole. Kwa upande wa wanawake wasiozaa yaani tasa, kwa Wanyaturu wanawake k**a hao huaminika kwamba kizazi chao kimechafuka. Ili kumsafisha, hupatiwa dawa ya kusafisha kizazi kutoka kwa mganga.
Mara nyingi walifanikiwa kuzaa na kikubwa iliaminika kwamba kutozaa ni mchezo wa kichawi. Ingawa maendeleo ya sayansi yanaonesha kuwa uzazi unaweza usifanyike kutokana na baba kuwa na matatizo, lakini kwa Wanyaturu mama ndiye alikuwa akinyooshewa kidole kunapotokea familia kukosa mtoto.
Wanyaturu wanathamini mwanamke anapozaa watoto wengi wakiamini, kuwa familia hiyo ina baraka nyingi za Mwenyezi Mungu ambazo huonekana kwa watoto wengi, na kwamba mtu huyo hupendwa na Mungu. Thamani nyingine ya watoto inatokana na kuamini kuwa ukoo huenea kwa haraka na kudumu kwa muda mrefu au kuendelea kwa kuwa na watoto wengi.
Kadhalika, kwa Wanyaturu kuwa na watoto wengi wa kiume kulionesha kupata ulinzi bora na wa kudumu katika familia. Pia mtoto wa kiume kwa Wanyaturu alichukuliwa kuwa ndiye atakayewatunza wazazi kuliko mtoto wa k**e, mlinzi wa familia yote na ndiye atakayeimarisha ukoo.
Kwa upande wa mama aliyezaa mapacha, hali ilikuwa tofauti, kwani anapojifungua mapacha hupigwa vigelegele (vinavyotokana na mlio baada ya kugongwa majembe) na huimbwa nyimbo fulani. Pia mzazi wa mapacha alifanyiwa karamu rasmi ambayo hujulikana k**a ‘Imma’.
Karamu hii hufanywa na wazazi au wajomba wa mama aliyejifungua wanapoenda kumpa pole kwa kumpelekea mbuzi na pombe ya asali.
Sherehe hiyo huishia kwa mume kutoa ng’ombe na kuwapa waliofanya sherehe hiyo. Hii ni tofauti sana na baadhi ya makabila ya Kiafrika ambayo miaka ya nyuma yaliona kuzaa mapacha k**a uchuro ambapo wengine waliuawa.
Utunzaji wa mtoto Utunzaji na malezi ya watoto kwa Wanyaturu ulitofautiana kulingana na jinsi ya mtoto. Apozaliwa mtoto wa kiume, watu walikata miti na kumletea nyumbani, hii ni kuonyesha kuwa atakuwa mjengaji wa nyumba na atakuwa na z**i la ng’ombe.
Pili mtoto wa kiume aliyezaliwa alikatiwa upinde kuonesha kuwa ni shujaa ambaye atalinda na kupigania nchi yake mpaka kufa.
Tatu wa kiume aliapishwa kuonesha kuwa yeye ni mtawala wa nyumba na familia yake. Kwa upande wa msichana alipozaliwa wanawake wa jamii hiyo walimkatia mzigo wa kuni kwa sababu ndiyo itakayokuwa kazi yake kubwa wakati atakapokuwa mtu mzima na mama mwenye mji. Kwamba jiko ilikuwa ndio ‘ofisi’ ya mtoto wa k**e ili familia iweze kula.