01/04/2026
Naitwa Vumilia Mariki, mkazi wa Uru, Moshi mkoani Kilimanjaro. Naomba msaada wa matibabu kwa mwanangu Levina John mwenye umri wa miaka sita (06), anayesumbuliwa na tatizo la miguu kupinda lililomfanya ashindwe kutembea kabisa.
Levina alizaliwa akiwa mzima na alianza kukua k**a watoto wengine. Alitambaa, akasimama na hatimaye akaanza kutembea bila shida yoyote. Hata hivyo, alipofikisha umri wa miaka minne, miguu yake ilianza kupinda taratibu, hali iliyozidi kuwa mbaya kadri siku zilivyopita hadi kufikia hatua ya kushindwa kutembea kabisa.
Kutokana na hali ngumu ya maisha, sikuweza kumpeleka hospitali mapema na badala yake nilijikuta nikimpeleka kwenye maombezi huku nikiendelea kumtumainia Mungu. Licha ya ushauri kutoka kwa baadhi ya watu kumpeleka kwa waganga wa kienyeji, nilikataa na kuendelea kutafuta msaada wa matibabu sahihi.
Baadaye nilifanikiwa kupata msaada wa shilingi 600,000 kupitia kikundi cha “Sadaka Yetu”, jambo lililonisaidia kumpeleka Hospitali ya Mawenzi kwa uchunguzi. Baada ya vipimo, madaktari waligundua kuwa Levina ana ugonjwa unaoitwa Blount’s disease, ambao husababisha ukuaji usio wa kawaida wa mfupa wa mguu na kupelekea kupinda kwa miguu.
Nilipatiwa rufaa ya kwenda CCBRT jijini Dar es Salaam kwa matibabu zaidi. Kwa msaada wa msamaria mwema, nilifanikiwa kufika huko pamoja na mwanangu.
Madaktari walieleza kuwa ili Levina aweze kusimama na kutembea tena, anahitaji kufanyiwa jumla ya operesheni nne (4), mbili kwa kila mguu. Kila operesheni inagharimu shilingi 1,200,000, hivyo kufanya jumla ya gharama kuwa shilingi 4,800,000.
Mpaka sasa, operesheni moja tayari imefanyika kwa msaada wa msamaria huyo. Hata hivyo, bado zinahitajika operesheni tatu zaidi—moja kukamilisha mguu uliokwisha anza kufanyiwa matibabu na mbili kwa mguu mwingine. Jumla ya fedha zinazohitajika kwa sasa ni shilingi 3,600,000.
Kwa unyenyekevu mkubwa, naomba msaada kutoka kwa watu wenye mapenzi mema ili kumsaidia mwanangu apate matibabu haya muhimu. Madaktari wamenihakikishia kuwa akipata matibabu haya kikamilifu, anaweza kurejea katika hali ya kawaida na kuanza kutembea tena.
Naomba msaada wenu ili kumuokoa Levina na ulemavu wa kudumu. Mungu awabariki wote watakaoguswa na kuchangia.